Tuesday, April 3, 2018

KITAMBI KINAVYOATHIRI NGUVU ZA KIUME NA AFYA KWA UJUMLA

Madhara ya kitambi



Unajitazama katika kioo, lakini unachukizwa! Unachukizwa na mwili wako mwenyewe. Hauna la kufanya, unabaki kuhuzunika tu.

Tumbo! Tumbo!


Naam, tumbo lako linaonekana kutuna na kutengeneza mkunjo. Linaonekana kwamba linaweza kuchukua muda mrefu sana kuwa katika hali hiyo, inaweza kuwa miezi au miaka; au linaweza lisiishe kabisa!

Licha ya kuwa tumbo kubwa linaweza kuufanya mwili kuwa na muonekano mbaya usiopendeza, kwa hakika madhara yake kiafya ni makubwa zaidi kuliko ubaya wa sura yenyewe.

Katika lugha yetu ya Kiswahili, mafuta ya tumboni hujulikana kama “kitambi.” Lakini pia kuna majina mengi ya utani yanayotumika mtaani kukiita hicho kitambi, baadhi ya majina ni kama vile tumbo la mtungi, kishikio cha mapenzi, tairi la akiba, tumbo la bia, friji n.k.

Kwa nini watu walipachika majina kama hayo?

Katika miongo michache ya nyuma hapa kwetu Tanzania, na hata katika baadhi ya nchi duniani; baadhi ya watu kutokana ukosefu wa elimu walivitazama vitambi kama dalili ya ustawi mzuri wa maisha, na hasa ndiyo sababu ya kuvitengenezea majina ya ziada.

Katika miaka ya hivi karibuni, watu wengi sana sasa wametambua vizuri kuwa kitambi ni tatizo kubwa la kiafya. Utawaona wako katika kumbi za michezo ya mazoezi ya viungo (gym), wengine wakiwa katika utaratibu maalumu wa chakula (dieting); na wengine wakiwa katika programu za tiba ili kupunguza mafuta hayo mwilini, na ikiwezekana kuyaondoa yote kabisa.

Hata hivyo, wapo baadhi ya watu bado wanauchapa usingizi. Hao bado wanafanya utani na mafuta!

Ndani ya kitambi kuna nini?

Ukweli wa mambo ulivyo, kitambi hakina utani! Ukileta utani katika mafuta hayo ya tumboni, basi muda si mrefu utagonga hodi katika chumba cha daktari ukiwa tayari na kisukari (TYPE 2), au ugonjwa wa moyo, au kupooza, au saratani, au shinikizo la damu la kupanda (High Blood Pressure), au matatizo ya kibofunyongo, au ugonjwa wa ini (cirrhosis) huku kuishiwa nguvu za kiume ikiwa ni jambo linalokwenda bega kwa bega na kitambi.

Je, hapo utaendelea kufanya utani na kitambi? Bado utaita tumbo la bia? Au kadha wa kadhaa? Hakika utakiita ni tumbo la kifo!

Hayo siyo mafuta mazuri kabisa, wala siyo mafuta ya kuyatania wala kuyachekelea! Ukiyafungulia mlango tu na kuyaruhusu yaweke maskani yake tumboni mwako, ni sawa na kuruhusu nyoka kukaa chumbani mwako, hatima yake ni nini? Bila shaka ni kung’atwa! Kama zisipofanyika juhudi za haraka za kuidhibiti sumu ya nyoka huyo, basi matokeo yaweza kuwa kifo! Kitambi pia, ni vivyo hivyo.

Wakati mafuta mengi yanapokuwa mwilini huleta tatizo. Lakini mafuta haya ya tumboni yana hatari kubwa zaidi hata kama ni madogo.

Baadhi ya watu kwa kutojua madhara ya vitambi, huchukulia mambo kwa wepesi, husema, “Tumbo langu ni dogo tu, ni kama halipo vile!”

Kwa mtazamo wao, ni kwamba wanaweza kunusurika na madhara ya kitambi.

Ni kweli kwamba, watu wanatofautiana ukubwa wa matumbo. Kuna ambao matumbo yao ni madogo, au ndio yanaanza. Kuna wengine ni makubwa kiasi, na wengine makubwa zaidi kiasi ambacho huwafanya kupata taabu sana katika kufanya kazi mbalimbali.

Lakini, ukweli wa mambo ulivyo ni kwamba, mafuta ya tumboni yanaweza kukuletea maradhi hata kama hauna uzito mkubwa au hauna tumbo kubwa.

Kwa nini mafuta ya tumboni yalete maradhi? Yana uhusiano gani na maradhi? Kwa nini yapunguze nguvu za kiume? Haya ni baadhi ya maswali ambayo yanaweza kugonga katika akili ya msomaji.

Ukweli ni kwamba, tumbo kubwa ni matokeo ya mafuta mengi mno yaliyoweka makazi yake ndani kabisa ya tumbo au fumbatio (abdomen) na kitabibu yanajulikana kama, “visceral fat.” Mafuta hayo huzonga na kudhuru figo zako, ini na viungo vingine vilivyo tumboni na kuharibu utendaji wa kazi wa viungo hivyo na kuvuruga utendaji wa homoni.

Ni mafuta ambayo huleta madhara makubwa katika mishipa yako ya damu. Seli za mafuta hayo huzalisha homoni na sumu ambazo moja kwa moja huathiri afya na tabia yako.

Aina ya mafuta yaliyo ndani ya kitambi

Lakini, kabla hatujaenda kuangazia kwa undani uhusiano wa kitambi na magonjwa mbalimbali ikiwa ni pamoja na upungufu wa nguvu za kiume ambacho ndiyo kilio cha wanaume wengi wenye vitambi, kwanza ni muhimu tufafanue kwa ufupi aina za mafuta yaliyo tumboni.

Tumboni kuna mafuta ya aina mbili. Aina ya kwanza ni mafuta yanayotokea chini ya ngozi ya tumbo. Mafuta haya unaweza kuyagusa kwa nje kwa kufinya ngozi ya tumbo. Mafuta haya hayana madhara yoyote na yana msaada mkubwa kwa viungo vilivyo ndani ya tumbo, hukaa kama mto (cushion) kwa viungo kujiegemeza. Kitabibu mafuta haya huitwa, “Subcutaneous fat.”

Aina ya pili ya mafuta, ni mafuta ambayo kitabibu huitwa, “Visceral fat,” ambayo tumekwishayataja mwanzoni mwa makala hii. Haya ni mafuta ambayo hukaa ndani kabisa ya tumbo, hujitengenezea makazi yake karibu kabisa na ini na viungo vingine viliomo tumboni. Mafuta haya ndiyo tatizo na chanzo cha matatizo mengi ya kiafya katika mwili wako, na ndiyo mafuta tunayokwenda kujadili madhara yake katika makala haya, sababu ya kutokea kwake na ufumbuzi wake.

Kisukari

Moja ya madhara ya kitambi ni kwamba, huweza kumfanya mtu apate ugonjwa wa kisukari kwa urahisi zaidi. Kwa sababu mafuta ya kitambi kwa ujumla huzonga viungo ambavyo husaidia kurekebisha sukari ndani ya damu.

Pindi insulini inapolielekeza ini kuhifadhi sukari ya akiba kwa ajili ya nishati ya baadaye, ini lililozongwa ndani tishu za mafuta hushindwa kuitikia ipasavyo. Matokeo yake, sukari huweza kuanza kujazana ndani ya mishipa ya damu na hivyo kuleta madhara makubwa katika viungo na kukaribisha ugonjwa wa kisukari.

Hali hiyo kitabibu huitwa “insulin resistance” ambapo seli za mwili hugoma kukubali homoni ya insulini. Insulini ni homoni ambayo hutolewa na seli za kongosho zijulikanazo kama beta cells. Hizi seli hutawanyika katika kongosho lote katika vishada vidogo vidogo vinavyojulikana kama visiwa (islets) vya Longerhans. Kazi kubwa za insulini huelekezwa kwenye umetaboli wa usimamizi wa kabohaidreti (sukari) na wanga, mafuta na protini.

Insulini pia hurekebisha kazi za seli za mwili, ikiwa ni pamoja na ukuaji. Insulini ni muhimu sana kwa matumizi ya mwili kama nguvu. “Insulin resistance” ni hali ambayo seli za mwili hugoma kukubaliana na insulini. Hii inaweza kuwa ni hali ya kawaida kama kiwango cha insulini kimepunguzwa. Matokeo yake viwango vikubwa vya insulini huhitajika ili insulini kufanya kazi yake vizuri. Hivyo, kongosho hufidia kwa kujaribu kutoa insulini zaidi. Mgomo huu hutokea katika mwili kuitikia insulini yake yenyewe (endogenous) au pindi insulini inapokuwa inaingizwa kwa sindano (exogenous).

Katika “insulin resistance” kongosho hutoa insulini zaidi na zaidi mpaka kufikia wakati sasa haliwezi tena kutoa insulini ya kutosha kwa ajili ya mahitaji ya mwili, hivyo sukari ndani ya damu hupanda.

Mshtuko wa moyo

​Kitambi kina urafiki mkubwa na ugonjwa wa moyo. Pindi unapokula chakula, kiwango chako cha insulini ndani ya damu hupanda. Kadiri sukari inavyopanda, ndivyo pia insulini nyingi inavyotolewa na kongosho ili kuendelea kuifanya sukari isipande juu zaidi.

Punde tu baada ya insulini kufanya kazi yake ya kushushua viwango vilivyopanda vya sukari, ini huondoa insulini kutoka ndani ya damu.

Hata hivyo, mafuta yaliyo ndani ya mikondo ya ini, huzuia na kukinza seli za ini kuondoa insulini kutoka katika mikondo ya damu.

Kwa hali hiyo, watu ambao hutunza mafuta mengi tumboni, wajue pia hutunza mafuta mengi katika ini zao, hali ambayo mafuta hayo huzuia ini kuondoa insulini ndani ya damu na hivyo kusababisha kuwa na kiwango kikubwa cha insulini.

Ni kwamba unahitaji insulini kuzuia viwango vya sukari ndani ya damu kupanda juu, lakini insulini nyingi hubana mishipa ya ateri na kusababisha mshtuko wa moyo.

Vyakula vya mafuta na ukosefu wa mazoezi husababisha ongezeko la uzito. Hali hii huzifanya njia katika mishipa ya damu kuwa miembamba zaidi na kukakamaa, matatizo ambayo hujulikana kitaalamu kama atherosclerosis au arterioscloris. Huu ni mchakato wa kunenepa na kukamaa kwa kuta za ateri kubwa na ateri za ukubwa wa kati.

“Arterioscloris” ni hali ambayo husababisha kutokea kwa maradhi ya ateri za moyo (coronary artery) ikipelekea kwenye ugonjwa wa moyo unaosababisha maumivu kifuani (angina) na mshtuko wa moyo, kupooza, na maradhi ya mishipa ya damu. Hii hutokana na lehemu (cholesterol) na baadhi ya vitu kujijenga katika kuta za mishipa ya damu.

Kama ujenzi huo wa lehemu utatokea katika mishipa mikubwa ya ateri karibu na moyo itasababisha mshtuko wa moyo, na kama itatokea katika mishipa midogo ya damu inayokwenda kwenye uume, kama tutakavyoeleza baadaye, itasababisha kushindwa kusimama kwa uume. Hali hii ya kushindwa kusimama kwa uume, kitabibu ni dalili ya tahadhari ya awali ya matatizo ya moyo.

Vipengele vinavyoweza kusababisha “arterioscloris” ni pamoja na “insulini resistance,” lehemu mbaya (LDL), shinikizo la damu la kupanda (HBP), uvutaji sigara, na kisukari.

Mshtuko wa moyo mara nyingi hutokea pindi damu inapoganda na hivyo kuziba mtiririko wa damu kupitia ateri ya moyo (coronary artery). Huu ni mshipa wa damu unaojaza damu inayokwenda sehemu za misuli ya moyo. Mtiririko wa damu ulioingiliwa unaweza kudhuru au kuharibu misuli ya moyo.

Mshtuko wa moyo pia huitwa myocardial infarction. Ni ugonjwa ambao mtu anaweza kujikuta katika hatari kubwa. Hii ni kwa sababu mara nyingi watu huchanganya dalili zake kwa kuziona ni za ugonjwa mdogo na hivyo kuchelewa kupata matibabu.

Watu wenye vitambi wako katika hatari kubwa ya kupata matatizo ya moyo kuliko watu ambao hawana vitambi.


Ni kwa namna gani kitambi huathiri nguvu za kiume?

​Tumeona hapo juu kwa ucahe jinsi kitambi kinavyoathiri afya. Sasa tuangalie jinsi kitambi kinavyoathiri nguvu za kiume.

​Mzunguko wa damu

Kitambi kinaenda bega kwa bega na upungufu wa nguvu za kiume. Kwa nini? Kwa sababu kitambi huharibu mzunguko wa adamu. Tunahitaji mzunguko wa damu wenye afya kwa ajili ya damu hiyo kuingia ndani ya uume na kujaa. Kama damu ya kutosha haingii kwenye uume nguvu za kiume pia hupotea. Uume hauwezi kusimama vizuri.

Homoni

Kibaya zaidi ni kwamba kitambi hubadilisha homoni ya kiume iitwayo testosterone kuwa homoni ya kike estrogen. Hili hutokeaje? Ni hivi. Mafuta ya kwenye kitambi huzalisha kimeg’enya kiiwatcho aromatase, na hiyo aromatase ndiyo inayobadilisha homoni ya kiume ya testosterone kuwa homoni ya kike estrogen.

Mishipa ya neva

Mafuta yaliyo kwenye kitambi hudhuru mishapa laini inayohusika na usimamaji wa uume. Uzito mdogo hata wa shilingi kutokana na mafuta yaliyo kwenye kitambi huweza kudhuru mishipa ya neva inayosimamisha uume.

Tezidume

Mafuta yaliyo kwenye kitambi pia huaharibu utendaji wa tezidume iitwayo tezidume (prostate gland) kwa sababu uzito wa mafuta hayo huleta shida kwenye tezidume.

Misuli

Pia uzito wa mafuta ya kwenye kitambi hudhuru misuli iitwayo pelvic floor muscles. Hii ni misuli muhimu sana, iko chini ya nyonga. Inafanya kazi nyingi, baadhi ya kazi zake ni kusaidia kusimamisha uume kuwa imara kabisa, na pia kuzuia kufika kileleni haraka. Mafuta ya kwenye kitambi huidhikisha misuli hii na kuipa shida.
KITAMBI KINAVYOATHIRI NGUVU ZA KIUME NA AFYA KWA UJUMLA

No comments:

Post a Comment